Wednesday 26 February 2014

NMB YAENDELEA KUSOGEZA HUDUMA KARIBU ZAIDI KWA WATEJA WAKE

·         Hili ni tawi la ishirini kufunguliwa mkoani Dar es Salaam
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam,Bw. Meck Sadick akikata utepe kuashilia uzinduzi rasmi wa tawi la NMB Mandela Road .Kwanza kushoto ni Meneja wa NMB kanda ya Dar es salaam ,Bw. Salie Mlay na kwanza kushoto ni  Mkuu  wa kitengo cha Huduma kwa wateja wakubwa  NMB, Bw.Gerald Kamugisha wakishuhudia ufunguzi huu uliofanyika jana jijini Dar es salaam.


Dar es Salaam,NMB yazindua tawi jipya barabara ya Mandela mkoani Dar es Salaam.
Hili ni tawi la ishirini kufunguliwa katika mkoa wa Dar es Salaaam, na hii inafanya NMB kuwa benki yenye matawi mengi zaidi Tanzania, ikiwa na matawi zaidi ya 500 yaliyosambaa nchi nzima.
Tawi hili la NMB Mandela Road linaongeza wigo wa matawi ya NMB yaliyofunguliwa katika wilaya mbali mbali nchini ambayo yanalenga katika kuleta unafuu kwa wateja na kupata huduma za kibenki karibu yao huku wakiendelea na shughuli mbali mbali za kila siku.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa tawi hili, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Said Meck Sadik amesema tawi hili litasaidia sana wananchi na wafanyabiashara wa eneo hilo kupata huduma za kibenki kwa ukaribu zaidi.
“ Mkoa unavyoendelea kupanuka na biashara zinaongezeka pia, basi ni muhimu kwa mabenki kama NMB kusogeza huduma karibu zaidi na wateja wao” Alisema Sadik,  akiongezea “Binafsi nawashukuru NMB kwa kuleta tawi hili jipya litakaloongeza maendelea kwenye eneo hili na kukidhi mahitaji ya kibenki kwa wananchi.”
Meneja wa NMB kanda ya Dar es salaam,Bw.Salie Mlay akimwelezea jambo Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam (kwanza kushoto) ,Bw.Meck Sadick  kuhusiana na huduma mbalimbali zitolewazo na tawi jipya la NMB mandela Road.
Vilevile, Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Salie Andrew Mlay amesema anatarajia kuwa tawi hilo jipya litakidhi mahitaji ya ongezeko kubwa la wateja wa NMB.

“Tunajivunia kufungua tawi hili, wateja wetu wamekua wakiongezeka kila siku, hivyo hatuna budi bali kubuni mbinu mbalimbali zitakozotuwezesha kuwafikia wateja wetu karibu zaidi ili kuondoa msongamano kwenye matawi na pia kuokoa muda wa wateja ili waweze kutumia muda wao kujiendeleza zaidi.” anasema Salie.

Katika kusherehekea ufunguzi rasmi wa tawi hili, Benki ya NMB inatoa msaada kwa jamii inayoizunguka kwenye sekta ya Afya. Benki ya NMB imekabidhi msaada wa vifaa vya hospitali vyenye thamani ya shilingi milioni kumi ili kuunga mkono jitihada za serikali na wananchi katika kuboresha huduma katika sekta ya afya. Msaada huu unatolewa kwa hospitali ya Amana pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.  
Tawi hili la NMB Mandela Road, linatoa huduma mbali mbali za kibenki ikiwemo akaunti za akiba, mikopo  , huduma za fedha za kigeni, kukusanya mapato na kulipia kwa niaba  ya serikali na taasisi mbalimbali. Tawi hili litakua wazi kila  Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa mbili  na nusu asubuhi hadi saa kumi na nusu jioni ( 8:30 am - 4:30 pm ) na Jumamosi kuanzia saa mbili na nusu asubuhi hadi saa sita na nusu mchana (8:30 am - 12:30 pm), Jumapili na siku za sikukuu hakutakuwa na huduma ndani ya tawi hili.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam,Bw.Meck Sadick (kwanza Kulia) akimkabidhi sehemu ya msaada wa vifaa vya hosipitali Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana ,Dr Meshack Shimwela .Mashuka ya Hospitali pamoja na Vitanda vya wodi ya akina mama ni miongoni mwa vifaa vilivyotolewa .Makabidhiano haya yamefanyika jana wakati wa uzinduzi wa tawi la NMB mandela Road Katikati ni Meneja wa NMB kanda ya Dar es salaam, Bw.Salie Mlay.

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Bw. Meck Sadick akimpongeza Mganga mkuu wa Idara ya Magonjwa ya wanawake na Uzazi Hospitali ya Taifa Muhimbili ,Dr Mathew Kallanga baada ya kupokea msaada wa vifaa vya hospitali vilivyotolewa na Benki ya NMB wakati wa Uzinduzi wa Tawi la NMB Mandela Road  katikati ni Meneja wa NMB kanda ya Dar es salaam,Bw.Salie Mlay.

No comments:

Post a Comment