Thursday, 6 March 2014

Mwanaharakati Jane Magigita akabidhiwa tuzo ya Dk. Martin Luther King kwa kupigania haki za kisheria za wanawake

Mwanaharakati Jane Magigita(kulia) akipokea tuzo ya Dk. Martin Luther King kutoka kwa Kaimu balozi wa Marekani nchini Tanzania, Virginia Blaser.
Watu waliohudhuria tukio hilo wakiwemo Mwenyekiti Mtendaji wa IPP media, Dk. Reginald Mengi na Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhan ambao pia walishawahi kupokea tuzo hiyo awali.
 ..................................................................................................................................................
Kaimu Balozi Virginia M. Blaser, amtunukia Bi Jane Magigita-Milyango tuzo ya Dk. Martin Luther King kwa kupigania haki za kisheria za wanawake.

Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Virginia M. Blaser, alimtunukia Bi. Jane Magigita–Milyango tuzo ya Haki ya Dk. Martin Luther King kwa mwaka 2014 kwa kutambua jitihada zake kubwa za kutetea haki za kisheria za wanawake, hususan katika kukabiliana na tatizo la ukatili wa kijinsia na suala la urithi na matumizi ya ardhi kwa wanawake wa vijijini. Bi Magigita ni mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa asasi isiyo ya kiserikali  iitwayo Equality for Growth (EfG) iliyosajiliwa mwaka 2008.  Vile vile ni mwanzilishi na mjumbe wa bodi wa taasisi kadhaa za hapa nchini ikiwa ni pamoja na tawi la Tanzania la African Evangelical Enterprise (AEE-Tz) na Children's Dignity Forum (CDF).  Hali kadhalika Bi. Magigita ni mjumbe wa timu maalumu ya wataalamu kutoka katika taasisi zinazotoa msaada wa kisheria.

Tuzo ya Haki ya Dk. Martin Luther King, Jr. hutolewa kila mwaka na Balozi wa Marekani nchini Tanzania ili kuenzi maisha na mafanikio ya Dk. King na ya Mtanzania ambaye kama ilivyokuwa kwa Dk. King, amejitoa kwa dhati kuwahudumia na kuwapigania wengine.

Katika hotuba yake, Kaimu Balozi Blaser alimpongeza Bi. Magigita kwa maono, ujasiri na kujitoa kwake kwa dhati katika kukabiliana na vitendo vya uonevu na ukiukwaji wa haki:  “Bi Magigita anapaisha na kuzipa nguvu sauti za Watanzania wenzake ili nao waweze kudai haki zao kwa njia za amani. Katika kipindi cha miaka 13 iliyopita, Bi Magigita amekuwa akitoa huduma ya msaada wa kisheria kwa waathiriwa wa vitendo vya ukatili wa kijinsia moja kwa moja au kwa kupitia Vituo mbalimbali vya Msaada wa Kisheria. Kutokana na jitihada za Bi. Magigita wanawake hawa pamoja na watoto wao  wameweza kukataa uonevu unaoambatana na ukatili wa kijinsia. Kama ilivyokuwa kwa watu walioandamana na Dk. King wanawake hawa wamejenga ujasiri na uwezo wa kudai haki zao za kisheria kama raia walio chini ya sheria za taifa hili adhimu.”

Kaimu Balozi Blaser aliendelea kusema kuwa, kama ilivyokuwa kwa Dk. King, Bi Magigita haogopi kutumia mivutano iliyopo katika jamii kama fursa ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii husika.

No comments:

Post a Comment