RAIS KIKWETE ATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea
kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Waziri wa Fedha, Mheshimiwa
William Mgimwa, aliyekuwa pia Mbunge wa Jimbo la Kalenga (Mkoa wa Iringa)
kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Rais
Kikwete amesema kuwa taifa limempoteza Waziri Mgimwa katika kipindi lilipokuwa
linamhitaji zaidi kutokana na mchango wake mkubwa ambao amekuwa akiutoa kupitia
nafasi zake za Waziri wa Serikali na mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Kalenga.
Kifo
cha Mheshimiwa Mgimwa kimetangazwa mchana wa leo, Jumatano, Januari Mosi, 2014,
na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK) Balozi Ombeni Sefue kwa niaba ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika
tangazo lake, Balozi Sefue amesema kuwa Waziri Mgimwa ameaga dunia asubuhi ya
leo saa 5:20 (Saa za Afrika ya Kati) katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic ,
Pretoria, Afrika Kusini ambako amekuwa amelazwa kwa muda sasa.
Balozi
Sefue amesema kuwa maandalizi ya kuurudisha nyumbani mwili wa Waziri Mgimwa
yanafanywa na Serikali kwa kushirikiana na familia yake na kuwa taarifa zaidi
kuliko suala hilo zitatolewa baadaye kwa kadri zinavyopatikana na maandalizi
yanavyoendelea.
Katika
salamu zake kwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda na kwa familia ya Marehemu
Mgimwa, Rais Kikwete amesema: “Sina
maneno ya kutosha kuelezea mshtuko na huzuni yangu kubwa kufuatia taarifa za
kifo cha Mheshimiwa Mgimwa. Binafsi nimemtembelea mara mbili kwenye Hospitali
alikokuwa amelazwa na mara ya mwisho hali yake ilikuwa imeimarika. Tulizungumza
kwa kiasi cha dakika 10 hivi akanielezea nia yake na tamaa yake ya kurejea nyumbani
kwa sababu hali yake ilikuwa nzuri.”
Ameongeza
Mheshimiwa Rais Kikwete: “Sote tunajua mchango wake katika Serikali. Sote
tulitamani kuendelea kuwa naye, lakini haya ni mapenzi ya Mungu.”
“Napenda
kutoa pole nyingi na rambirambi zangu za dhati kwa wana-familia wote kwa
kuondokewa na mhimili wao. Naungana nanyi katika kuomboleza msiba huo mkubwa.
Napenda mjue kuwa msiba huu ni msiba wangu pia. Machungu yenu ni majonzi yangu,”
amesema Rais Kikwete.
Rais
pia amewatumia rambirambi wananchi wa Jimbo la Kalenga akisema kuwa wamempoteza
mwakilishi na mtetezi mahiri wa maslahi yao.
No comments:
Post a Comment