Saturday 18 January 2014

MNYIKA KUKUTANA NA WANANCHI WA PEMBEZONI YA BARABARA YA MOROGORO KESHO (19 JANUARI 2014)

Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), John Mnyika.
Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ubungo inatoa taarifa kwa umma kwamba John Mnyika (Mb) jumapili tarehe 19 Januari 2014 atakutana na wananchi wenye makazi pembezoni mwa Barabara ya Morogoro wanaothirika na nyongeza ya hifadhi kinyume cha sheria ya ardhi na amri ya Mahakama Kuu.

Mkutano huo wa Mbunge na wananchi utafanyika katika eneo la Luguruni Makondeko na utahusisha pia kamati ya waathirika wa hifadhi ya barabara pamoja na wananchi wengine kutoka maeneo mbalimbali ya majimbo ya Ubungo, Kisarawe na Kibaha.

Wananchi hao wamekuwa na malalamiko ya haki zao za msingi za makazi na za kibinadamu kuvunjwa kwa maagizo kutoka kwa Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli ambayo hutekelezwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) kinyume na sharia.
 
Aidha, kwa nyakati mbalimbali katika ya mwaka 2011, 2012 na 2013 yamejitokeza malumbano ndani na nje ya Bunge baina ya Mbunge Mnyika (akiwakilisha wananchi) na Waziri Magufuli (akisisitiza msimamo wa serikali) kuhusu utata wa upana wa barabara ya Morogoro na haki za wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni ya barabara hiyo.
Kwa upande mwingine, Malalamiko hayo ya wananchi yalishawahi kufikishwa katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kupitia shauri Na 80 la 2005 na hukumu kutolewa tarehe 31 Mei 2013, ambapo Mahakama Kuu ilitamka kuwa sheria ya The Highway Ordinance Cap 167 Government Notice No 161 of 5/5/1967 ambayo hutumiwa na Wizara ya Ujenzi na Tanroads kuingia katika ardhi  za wananchi “ni batili kwa kutofautiana na vifungu vya 15 na 16 vya Sheria ya Ardhi ya Vijiji na 5 ya 1999”.

Kamati ya waathirika wa hifadhi ya barabara imemwandikia barua mbunge kumweleza kuwa mahakama kuu imeamua kuwa  inayodaiwa na walalamikiwa (Wizara ya Ujenzi) kuwa ni hifadhi ya barabara (hadi Mita 121 kutoka katikati ya barabara ya Morogoro pande zote mbili), iligawiwa kwa walalamikaji kihalali kwa mujibu wa sheria za nchi wakati wa operesheni vijiji ya miaka 1970, na hivyo kwa mujibu wa vifungu vilivyotajwa hapo juu  ni mali halali ya wananchi.

Katika mkutano huo, mbunge atasikiliza malalamiko ya wananchi juu ya hatua ya Wizara ya Ujenzi na Tanroads bila kujali hukumu ya mahakama kuendelea kushikilia ardhi za wananchi zilizo nje ya mita 30 kutoka katikati ya barabara isivyo halali bila ya kulipa fidia stahili katika maeneo ambayo Serikali inataka kuyatwaa kwa ajili ya miundombinu na kuwazuia wananchi kuendeleza maeneo yao yaliyo nje ya mipango ya maendeleo ya umma.

Mbunge anakwenda kukutana na wananchi kwa kuzingatia kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria ya barabara namba 13 ya 2007, na Kanuni zake kupitishwa kupitia Tangazo la Serikali namba 21 la tar 23 Januari 2009. Kifungu cha 29, kinataja upana wa hifadhi za barabara kuu na za mikoa (Trunk and regional roads) utakuwa ni mita 60 tu, ikihusisha mita 30 kila upande kutoka katikati ya barabara”.
Aidha kifungu 27 A cha Kanuni hizo kinataja upana wa njia za barabara za lami (lanes), kwa barabara kuu (Trunk roads), kuwa hautakiwi kupungua Mita 3.25. Kwa maana hiyo hifadhi ya barabara ya mita 60 inaweza kutumika kujenga njia zinazohitajika. 
 
Maana yake ni kwamba  Wizara ya Ujenzi na Tanroads wanaweza kuheshimu maamuzi ya mahakama na sheria za nchi na kuwezesha barabara ya Morogoro kujengwa na kupanuliwa kwa njia za kutosha huku ikiacha eneo la ziada kwa ajili ya wananchi kuweza kujiendeleza na kuendeleza Jiji.

Hivyo, mkutano huo wa mbunge na wananchi utatoa nafasi ya hatua kupendekezwa zitakazowezesha kulindwa kwa haki za msingi za wananchi lakini pia kufanikisha maendeleo ya nchi kwenye sekta muhimu za ujenzi wa makazi na miundombinu.

Imetolewa tarehe 18 Januari 2014 na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ubungo:
Aziz Himbuka
Katibu Msaidizi

No comments:

Post a Comment