Dar es Salaam,NMB yazindua tawi jipya barabara ya Mandela mkoani Dar es Salaam.
Hili ni tawi la ishirini kufunguliwa katika mkoa wa Dar es Salaaam, na hii inafanya NMB kuwa benki yenye matawi mengi zaidi Tanzania, ikiwa na matawi zaidi ya 500 yaliyosambaa nchi nzima.
Tawi hili la NMB Mandela Road linaongeza wigo wa matawi ya NMB yaliyofunguliwa katika wilaya mbali mbali nchini ambayo yanalenga katika kuleta unafuu kwa wateja na kupata huduma za kibenki karibu yao huku wakiendelea na shughuli mbali mbali za kila siku.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa tawi hili, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Said Meck Sadik amesema tawi hili litasaidia sana wananchi na wafanyabiashara wa eneo hilo kupata huduma za kibenki kwa ukaribu zaidi.
“ Mkoa unavyoendelea kupanuka na biashara zinaongezeka pia, basi ni muhimu kwa mabenki kama NMB kusogeza huduma karibu zaidi na wateja wao” Alisema Sadik, akiongezea “Binafsi nawashukuru NMB kwa kuleta tawi hili jipya litakaloongeza maendelea kwenye eneo hili na kukidhi mahitaji ya kibenki kwa wananchi.”Vilevile, Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Salie Andrew Mlay amesema anatarajia kuwa tawi hilo jipya litakidhi mahitaji ya ongezeko kubwa la wateja wa NMB.
“Tunajivunia kufungua tawi hili, wateja wetu wamekua wakiongezeka kila siku, hivyo hatuna budi bali kubuni mbinu mbalimbali zitakozotuwezesha kuwafikia wateja wetu karibu zaidi ili kuondoa msongamano kwenye matawi na pia kuokoa muda wa wateja ili waweze kutumia muda wao kujiendeleza zaidi.” anasema Salie.
Katika kusherehekea ufunguzi rasmi wa tawi hili, Benki ya NMB inatoa msaada kwa jamii inayoizunguka kwenye sekta ya Afya. Benki ya NMB imekabidhi msaada wa vifaa vya hospitali vyenye thamani ya shilingi milioni kumi ili kuunga mkono jitihada za serikali na wananchi katika kuboresha huduma katika sekta ya afya. Msaada huu unatolewa kwa hospitali ya Amana pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Tawi hili la NMB Mandela Road, linatoa huduma mbali mbali za kibenki ikiwemo akaunti za akiba, mikopo , huduma za fedha za kigeni, kukusanya mapato na kulipia kwa niaba ya serikali na taasisi mbalimbali. Tawi hili litakua wazi kila Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa mbili na nusu asubuhi hadi saa kumi na nusu jioni ( 8:30 am - 4:30 pm ) na Jumamosi kuanzia saa mbili na nusu asubuhi hadi saa sita na nusu mchana (8:30 am - 12:30 pm), Jumapili na siku za sikukuu hakutakuwa na huduma ndani ya tawi hili.
No comments:
Post a Comment