Friday, 3 January 2014

Shehena ya meno ya Tembo yanaswa Dar

Meno ya Tembo
Shehena ya meno ya tembo ambayo bado haijajulikana idadi wala uzito wake, imekamatwa na maofisa wa Maliasili kwenye Bandari ya Dar es Salaam ikiwa ndani ya kontena.

Hata hivyo, waandishi wa habari ambao walifuatana na Kaimu Afisa Habari wa Wizara ya Maliasili na Utalii Tabu Nziku, jana kwenye Bandari hiyo ili wakashuhudie kukamatwa kwa meno hayo walizuiliwa kwa muda wa saa mbili na walinzi wa Suma JKT kwa sababu ambazo hazijajulikana.


Licha ya kujitambulisha kuwa ni waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari, maafisa hao waliwazuia kufanya kazi yao, jambo lililozusha mjadala na mabishano kwa muda mrefu pamoja na kuwepo kwa maofisa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.


Huku mabishano hayo yakiendelea walinzi hao walikuwa wanashinikiza waandishi wa habari watolewe nje, pamoja na kuwa wakati huo walikwishaingia ndani, na kugoma katakata kuwaonyesha kontena hilo.


Kaimu Mrugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande, alithibitisha kuwapo kwa kontena hilo lenye meno ya tembo, lakini alisema yeye hana uwezo wa kulizungumzia suala hilo bali wenye mamlaka hiyo ni Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara.


Aliongeza kuwa kwa sasa anafanya mawasiliano na ngazi hizo za juu na atakapokuwa tayari atamjulisha Afisa Habari ili awaite waandishi kwa ajili ya kulizumgumzia suala hilo.


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu, alisema amezipata taarifa hizo, lakini kwa muda huo alikuwa njiani akitokea Maswa na kwamba wizara inaandaa taarifa rasmi ili kulizungumzia jambo hilo ambayo itasambazwa kwenye vyombo vya habari.


Hata NIPASHE ilipomtafuta Kamanada wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, simu yake ya mkononi ilipokelewa na msaidizi wake ambaye alisema kuwa Kamishna Kova alikuwa katika kikao.


Matukio ya kuuawa kwa tembo yamekithiri nchini na hivi karibuni, Rais Jakaya Kikwete alisema kuwa sensa ya ndovu katika Pori la Hifadhi ya Selous imekamilika, lakini taarifa yake inatisha kwani kuna ndovu 13,084 tu wakati mwaka 1976 walikuwepo tembo 109,419.


Aliongeza kuwa watu 1,030 walikamatwa pamoja na silaha za kijeshi 18, za kiraia 1579, na shehena kubwa za meno ya tembo na nyara nyingine navyo vilikamatwa, na watu kadhaa wameshafikishwa mahakamani na kwamba awamu ya pili ya Operesheni Tokomeza Ujangili itaanza.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment