Thursday, 30 January 2014

Mwanafunzi wa Ardhi atoa changamoto kwa vijana kupitia kitabu chake cha 'Safari Ya Ndoto'

 
Mtunzi wa kitabu cha 'Safari Ya Ndoto' Bw. Aman Nguku (kulia) ambaye pia ni mwanafunzi wa chuo cha Ardhi akiwaelezea waandishi wa habari na wageni waalikwa (hawapo pichani) kuhusu kitabu hicho alichokizindua jana jijini Dar es Salaam. (Picha Zote na Atuza Nkurlu)
Nguku anaelezea kwamba kitabu hicho yenye kauli mbiu “Sio Serikali ni Mimi, Wewe na Sisi,” inatoa hamasa kwa watu hasa hasa kundi la vijana waweze kuwa na uthubutu wa kutimiza malengo yao katika maisha. Wanaoshuhudia ni mama yake mkubwa Bi. Anna Kikwa na baba yake mdogo Bw. Emmanuel Mallewo.
Bi. Kikwa (kushoto) na Bw. Mallewo wakionyesha kitabu cha 'Safari Ya Ndoto' alichokiandika mwanao Aman (katikati) anayesoma shahada ya uchumi mwaka wa tatu katika chuo kikuu cha Ardhi.
Mtunzi wa kitabu cha 'Safari Ya Ndoto' Aman Nguku akihojiwa na waandishi wa habari katika uzinduzi wa kitabu hicho jana. Wanaoshuhudia ni walezi wake Bi. Kikwa na Bw. Mallewo.
.............................................................................................
 
Vijana wakitanzania wameaswa kuacha kulalamika na kuishi katika maisha ya nadharia, badala yake wameshauriwa kubadilika kuwa watendaji na wenye uthubutu wa kutimiza malengo yao katika maisha.
 
Maneno hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Amajat Investment Bw. Aman Nguku  jijini Dar es Salaam jana katika uzinduzi wa kitabu chake kiitwacho ‘Safari Ya Ndoto’ inayobeba kauli mbiu “Sio Serikali ni Mimi, Wewe na Sisi.”
 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Bw. Nguku alisema imefika wakati sasa watanzania hasahasa kundi la vijana waamke kutoka usingizini na kutimiza malengo yao ya kimaisha ambayo wanapenda kufikia.
 
“Imetosha kusema kesho, kufikiri bila kutenda na kuongea bila vitendo. Kinachotakiwa ni kuanza utekelezaji,” alinukuu Bw. Nguku kutoka kwenye kitabu chake chenye kurasa 108.

Akielezea madhumuni ya kuandika kitabu hicho, Bw. Nguku ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu anayesomea shahada ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Ardhi jijini Dar es Salaam alisema:

“Hiki kitabu ni mahususi kwa wale watu ambao wana ndoto mbali mbali katika maisha yao lakini hawajui pakuanzia, iwe ndoto ya kuwa mfanyabiashara maarufu, mwanasiasa au daktari bingwa. Hiki kitabu ni ramani maalum kwao.”

Aliendelea, “Kitabu hiki kinaweza pia kuwa changamoto kwa wale ambao wamekata tamaa katika maisha. Kwa kusoma maandishi ya kitabu hiki, wanaweza wakafufua ndoto zao na kufanikiwa katika yale waliyoyapanga.”

‘Safari Ya Ndoto’ pia inabeba dondoo kutoka kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, mfanyabiashara maarufu Bw. Reginald Mengi na Mkurugenzi Mtendaji wa Helvetic Solar Contractors Bw. Patrick Ngowi.
 
Kitabu hiki kinasambazwa katika maduka mbali mbali jijini Dar es Salaam na nchi nzima ili watanzania wengi wapate kukisoma. Kinauzwa kwa Tsh 5000 tu.
Kwa sasa, mtunzi Nguku pia anaandika vitabu vingine viwili venye vichwa ‘Ndogo lakini muhimu, kesho’ na ‘What is life for!(Maisha ni ya nini!).

No comments:

Post a Comment